24 Halafu kati ya makuhani waliokuwa viongozi nilichagua kumi na wawili: Sherebia, Hashabia pamoja na wenzao kumi.
25 Hawa niliwapimia kwa mizani fedha, dhahabu na vyombo ambavyo mfalme, washauri wake, maofisa wake pamoja na watu wa Israeli walivyokuwa wamevitoa kwa ajili ya sadaka ya nyumba ya Mungu wetu.
26 Hivi ndivyo vitu nilivyowapimia: Fedha tani 22, vyombo 100 vya fedha, uzito wake kilo 70, dhahabu kilo 3400,
27 mabakuli 20 ya dhahabu, uzito wake kilo 8, vyombo viwili vya shaba nzuri iliyongaa yenye thamani kama ya dhahabu.
28 Kisha nikawaambia, “Nyinyi ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Kadhalika vyombo ni wakfu na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu.
29 Tafadhali vilindeni na vitunzeni mpaka mtakapovipima mbele ya makuhani wakuu, Walawi na viongozi wa koo za Israeli, huko Yerusalemu katika vyumba vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”
30 Basi, makuhani na Walawi wakachukua fedha, dhahabu na vyombo vyote walivyopimiwa, ili kuvipeleka mjini Yerusalemu katika nyumba ya Mungu wetu.