Ezra 9:7-13 BHN

7 Tangu nyakati za babu zetu hadi sasa, sisi watu wako tumekukosea sana. Na kwa sababu ya dhambi zetu, sisi, wafalme wetu na makuhani wetu tumetiwa mikononi mwa wafalme wa nchi za kigeni, tukauawa, tukachukuliwa mateka na kunyanganywa mali zetu. Na hadi hivi leo, tumetiwa haya kupita kiasi.

8 Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa muda mfupi umetuonesha huruma yako na kuwawezesha baadhi yetu kuponyoka kutoka utumwani na kuishi kwa usalama mahali hapa patakatifu. Badala ya utumwa, umetupa furaha na maisha mapya.

9 Hukutuacha tuishi utumwani ingawa tulikuwa tu watumwa Uliwafanya wafalme wa Persia wawe wema kwetu na kuturuhusu tuishi na kuijenga nyumba yako iliyokuwa imebomoka, ukatufanya tukae salama hapa Yuda na Yerusalemu.

10 “Lakini sasa, ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo yote? Maana, tumeziasi amri zako

11 ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii ukisema: ‘Nchi mnayoiendea na ambayo itakuwa mali yenu ni nchi iliyo najisi yenye uchafu wa wakazi toka nchi mbalimbali, kwa machukizo yao, wameijaza unajisi tele kila mahali.

12 Kwa hiyo, msiwaoze watu hao binti zenu, wala msiwaruhusu wavulana wenu kuwaoa binti zao. Pia, msishughulikie usalama au mafanikio yao, ili nyinyi wenyewe muweze kuwa na nguvu, na mfaidi mema ya nchi hiyo na kuwaachia watoto wenu kama urithi milele.’

13 Hata baada ya yote yaliyotupata kwa sababu ya maovu yetu na makosa yetu mengi, tunajua kwamba adhabu uliyotupa, ee Mungu wetu, ni ndogo ikilinganishwa na makosa yetu, na umewaacha baadhi yetu hai.