3 Zivunjilieni mbali madhabahu zao na kuzibomoa kabisa nguzo zao. Ziteketezeni kwa moto sanamu zao za Ashera na kuzikatakata sanamu zao za kuchonga na kufutilia mbali jina lao na mahali hapo.
4 “Wala msimwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, namna hiyo yao.
5 Bali mtakwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atachagua katika makabila yote ili kuliweka jina lake na makao yake hapo; huko ndiko mtakakokwenda.
6 Huko mtapeleka tambiko zenu za kuteketezwa na sadaka zenu, zaka zenu za matoleo yenu, sadaka zenu za nadhiri, matoleo yenu ya hiari na wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu.
7 Huko, mtakula mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na mtafurahi nyinyi pamoja na watu wa nyumbani mwenu kwa ajili ya mafanikio yenu aliyowabarikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
8 “Msifanye kama tunavyofanya sasa, kila mtu kama apendavyo mwenyewe;
9 kwa sababu bado hamjaingia mahali pa kupumzikia na katika urithi anaowapeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.