15 Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa huko Misri na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwakomboa; ndiyo maana leo nawaamuru hivyo.
16 Lakini akikuambia, ‘Sitaondoka kwako,’ kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako na anaridhika kuishi nawe,
17 basi, utachukua shazia na kutoboa sikio lake mpaka hiyo shazia iingie mlangoni naye atakuwa mtumwa wako milele. Kadhalika mtendee vivyo hivyo mtumwa wako wa kike.
18 Wala usione ugumu utakapomwacha huru mtumwa wako, maana, amekutumikia kwa muda wa miaka sita kwa nusu ya ujira wa mtumishi wa kuajiri. Fanya hivyo, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakubariki kwa kila utakalofanya.
19 “Mtolee Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa kundi lako la ng'ombe na kondoo. Usiwafanyize kazi ng'ombe hao na kondoo hao usiwakate manyoya.
20 Kila mwaka, wewe na jamaa yako mtakula wanyama hao mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua.
21 Lakini mnyama huyo akiwa na dosari yoyote, yaani akiwa kilema au kipofu, au ana kasoro yoyote kubwa, usimtoe kuwa sadaka kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.