1 “Adhimisheni mwezi wa Abibu na kufanya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana katika mwezi huo wa Abibu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwatoa Misri wakati wa usiku.
2 Mtatoa sadaka ya Pasaka kutoka mifugo yenu ya kondoo au ng'ombe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atachagua likae jina lake.
3 Msile sadaka hiyo na mikate iliyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso – kwa sababu mlitoka Misri kwa haraka; kwa hiyo, muda wote mtakaoishi mtakumbuka ile siku mlipotoka Misri.
4 Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi.
5 Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa,
6 bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri.