4 maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayekwenda pamoja nanyi kupigana kwa niaba yenu dhidi ya adui zenu na kuwapa ushindi.’
5 “Kisha maofisa watawaambia watu: ‘Kuna mtu yeyote hapa aliyejenga nyumba mpya lakini hajaizindua? Arudi nyumbani, asije akafia vitani na mtu mwingine akaizindua.
6 Kuna mtu yeyote hapa aliyepanda mizabibu na ambaye hajafurahia matunda yake ya kwanza? Arudi nyumbani asije akafia vitani na mtu mwingine akafurahia matunda yake.
7 Kuna mwanamume yeyote hapa aliyeposa na yuko karibu kuoa? Arudi nyumbani, asije akafia vitani, na mwanamume mwingine akaoa mchumba wake.’
8 Maofisa wataendelea kuwaambia watu, ‘Je, yupo hapa mtu aliyekufa moyo? Arudi nyumbani, asije akasababisha wenzake kufa moyo kama yeye.’
9 Maofisa wakisha sema na watu, basi makamanda watawaongoza watu.
10 “Mnapokaribia mji kuushambulia, kwanza wapeni wakazi wake masharti ya amani.