17 “Msipotoshe haki za wageni na yatima. Wala msichukue vazi la mjane kuwa rehani.
18 Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Kwa hiyo ninawapeni amri hiyo.
19 “Mnapovuna mavuno yenu shambani na kusahau masuke mengine humo, msirudi kuyachukua, ila waachieni wageni, yatima na wajane, ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu awabariki katika kazi zenu zote.
20 Mkipukutisha mizeituni yenu kuvuna matunda, msirudi kupukutisha tena vitawi vyake, ila waachieni wageni, yatima na wajane.
21 Mnapochuma zabibu, msirudi kuokota zabibu zilizobaki ila waachieni wageni, yatima na wajane.
22 Mtakumbuka kuwa nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri; kwa hiyo ninawapeni amri hii.