46 Lakini hizo zitakuwa ushahidi wa hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwenu na wazawa wenu milele.
47 “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwabariki katika kila njia, lakini nyinyi hamkumtumikia kwa moyo wa furaha na mkunjufu.
48 Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize.
49 “Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi.
50 Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana;
51 litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize.
52 Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni.