48 Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize.
49 “Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi.
50 Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana;
51 litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize.
52 Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni.
53 Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni.
54 Hata mtu mpole kabisa na aliyelelewa vizuri sana atamnyima chakula ndugu yake, mkewe ampendaye na mtoto wake atakayesalia;