3 Maana nitalitangaza jina la Mwenyezi-Mungu,nanyi mseme, ‘Mungu wetu ni Mkuu’.
4 “Mwenyezi-Mungu ni Mwamba wa usalama;kazi zake ni kamilifu,njia zake zote ni za haki.Yeye ni Mungu mwaminifu asiye na kosa,yeye hufanya mambo ya uadilifu na ya haki.
5 Lakini nyinyi mmekosa uaminifu kwake,nyinyi sio watoto wake tena kwa sababu ya uovu,nyinyi ni kizazi kiovu na kipotovu.
6 Mnawezaje kumlipa hivyo Mwenyezi-Mungu,enyi watu wapumbavu na msio na akili?Je, yeye siye Baba yenu aliyewaumba,aliyewafanya na kuwaimarisha?
7 Kumbukeni siku zilizopita,fikirieni miaka ya vizazi vingi;waulizeni baba zenu nao watawajulisha,waulizeni wakubwa wenu nao watawaeleza.
8 Mungu Mkuu alipoyagawia mataifa mali yao,alipowagawa wanadamu,kila taifa alilipatia mipaka yake,
9 kulingana na idadi ya watoto wa Mungu,lakini alijiwekea watu wa Yakobo kuwa wake,hao alijichagulia kuwa mali yake.