1 “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafikisha kwenye nchi ambayo mtakwenda kufanya makao yenu na atayafukuza mataifa mengi kutoka nchi hiyo. Mtakapoingia, atayafukuza mbele yenu mataifa saba makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi: Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
2 Pia, baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuyatia mikononi mwenu, mkawashinda watu hao na kuwaangamiza kabisa, msifanye agano lolote nao wala msiwahurumie.
3 Msioane nao, wala msiwaoze binti zenu au wana wenu kwao.
4 Mkifanya hivyo wao watawapotosha watoto wenu wasimfuate Mwenyezi-Mungu, na kuwafanya waabudu miungu mingine, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, halafu atawaangamiza mara moja.
5 Lakini watendeni hivi: Mtazivunjilia mbali madhabahu zao na kuzibomoa nguzo zao. Na sanamu za Ashera mtazikatilia mbali na kuzitia moto sanamu zao za kuchonga.
6 Fanyeni hivyo kwa kuwa nyinyi mmewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kati ya watu wote ulimwenguni aliwachagua nyinyi ili muwe taifa lake mwenyewe.