10 Lakini huwalipa wanavyostahili wale wanaomchukia, wala hatasita kuwaadhibu wanaomchukia.
11 Kwa hiyo muwe waangalifu kushika amri, masharti na maagizo ninayowaamuru leo.
12 “Mkisikiliza maagizo haya na kuyashika hata kuyatenda, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atashika agano lake nanyi na atawaonesheni fadhili kama alivyowaahidi babu zenu.
13 Atawapenda na kuwabariki, nanyi mtaongezeka na kuwa na wazawa wengi; atayabariki mashamba yenu ili mpate nafaka, divai na mafuta; atawabariki kwa kuwapeni ng'ombe na kondoo wengi katika nchi aliyowaahidi babu zenu kuwa atawapeni nyinyi.
14 Mtabarikiwa kuliko watu wengine wote ulimwenguni. Miongoni mwenu hakutakuwa na mwanamume wala mwanamke tasa.
15 Mwenyezi-Mungu atawaondoleeni magonjwa yote na hamtapatwa na magonjwa yoyote ya kutisha kama yaliyowapata huko Misri, lakini atawapa maadui zenu magonjwa hayo.
16 Angamizeni taifa lolote ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; atalitia mikononi mwenu, wala msilionee huruma. Msiabudu miungu yao, kwani jambo hili litakuwa mtego kwenu.