1 Lifuatalo ni simulizi la Nehemia, mwana wa Hakalia.Ikawa, nilipokuwa katika mji mkuu wa Susa, katika mwezi wa Kislevu wa mwaka wa ishirini,
2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akaja pamoja na baadhi ya watu toka nchini Yuda. Nikawauliza kuhusu Wayahudi wenzetu waliosalimika, yaani ambao hawakuhamishiwa Babuloni na kuhusu mji wa Yerusalemu.
3 Wao wakaniambia, “Wayahudi waliosalimika na kubaki katika mkoa ule, wako katika taabu na aibu. Ukuta wa mji wa Yerusalemu umebomolewa na malango yake yameteketea.”
4 Niliposikia hayo nilikaa chini na kulia, nikaomboleza kwa siku kadhaa. Nikafunga na kumwomba Mungu wa mbinguni,
5 nikisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbinguni, wewe u Mungu aliye mkuu na wa kutisha, unalishika agano lako na unawafadhili wale wakupendao na kuzishika amri zako.