Nehemia 2 BHN

Nehemia anakwenda Yerusalemu

1 Katika mwezi wa Nisani, katika mwaka wa ishirini wa utawala wa mfalme Artashasta, wakati divai ilipokuwa mbele yake, nilichukua divai na kumpelekea mkononi mwake. Kamwe sikuwahi kuwa mwenye huzuni mbele yake.

2 Mfalme Artashasta akaniuliza, “Je, mbona unaonekana kuwa mwenye huzuni, ingawa huonekani kuwa mgonjwa? Naona una huzuni sana moyoni mwako!” Ndipo nilipoogopa sana.

3 Nikamjibu, “Ee mfalme, udumu milele! Kwa nini nisiwe mwenye huzuni wakati mji wa Yerusalemu yalimo makaburi ya babu zangu uko tupu na malango yake yameteketezwa kwa moto?”

4 Ndipo mfalme Artashasta akanijibu, “Sasa unaomba nini?” Nikamwomba Mungu wa mbinguni.

5 Halafu nikamwambia mfalme, “Ee mfalme, ikiwa unapendezwa nami na ikiwa nimepata upendeleo mbele yako, nakuomba unitume Yuda ili niende kuujenga upya mji ambamo yamo makaburi ya babu zangu.”

6 Mfalme akaniuliza (malkia akiwa karibu naye), “Utakuwa huko kwa muda gani na utarudi lini hapa?” Ombi langu akalikubali nami nikamjulisha wakati nitakaporudi.

7 Nikamjibu, “Ee mfalme ikiwa unapendezwa nami, naomba nipewe barua ili nizipeleke kwa watawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate ili waniruhusu nipite hadi nchini Yuda.

8 Pia nakuomba barua iandikwe kwa Asafu mtunzaji wa msitu wa kifalme ili anipatie mbao za kutengenezea miimo ya malango ya ngome ya hekalu, ukuta wa mji na nyumba yangu nitakamokaa.” Mfalme akakubali ombi langu kwa kuwa Mungu, kwa wema wake, alikuwa pamoja nami.

9 Nilipowafikia wakuu wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, niliwapa barua za mfalme. Mfalme alikuwa amenituma pamoja na maofisa wa jeshi na wapandafarasi.

10 Lakini Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, Mwamoni, mtumishi wake, waliposikia kuwa nimekuja ili kushughulikia hali njema ya watu wa Israeli, hawakufurahia kabisa jambo hilo.

11 Hivyo nikafika Yerusalemu, nikakaa huko kwa siku tatu.

12 Kisha niliondoka usiku, mimi pamoja na watu wachache; sikumwambia mtu yeyote yale ambayo Mungu alikuwa ameyaweka moyoni mwangu kwa ajili ya mji wa Yerusalemu. Lakini siku moja usiku, niliondoka na kuwachukua watu wachache tu. Sikuchukua mnyama yeyote isipokuwa punda niliyempanda mimi mwenyewe.

13 Nikatoka nikipitia Lango la Bondeni katika njia ielekeayo kwenye Kisima cha Joka na Lango la Mavi; nikazikagua kuta za mji wa Yerusalemu ambazo zilikuwa zimebomolewa pamoja na malango yake ambayo yalikuwa yameteketezwa kwa moto.

14 Halafu, nikaenda kwenye Lango la Chemchemi na kwenye Bwawa la Mfalme. Lakini yule punda niliyempanda hakuweza kupita.

15 Wakati huo wa usiku, nikapitia bondeni na kukagua ukuta wa mji. Nilirudi nikapitia Lango la Bondeni.

16 Maofisa hawakujua mahali nilipokuwa nimekwenda wala nimefanya nini. Tena nilikuwa sijawaambia Wayahudi, makuhani, viongozi, wakuu wala wale watu ambao wangeifanya kazi ya kuujenga upya mji.

17 Kisha nikawaambia, “Bila shaka mnaliona tatizo letu kuwa mji wa Yerusalemu ni magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Basi, na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu ili tusiaibishwe zaidi.”

18 Nikawaeleza jinsi Mungu alivyokuwa pamoja nami akinitendea kwa wema wake. Nikawaeleza pia maneno ambayo mfalme alikuwa ameniambia. Wao walipoyasikia hayo, wakasema, “Haya, na tuanze kazi ya ujenzi.” Hivyo wakajiandaa kwa kazi hiyo njema.

19 Lakini Sanbalati, Mhoroni, Tobia, Mwamoni mtumishi wake, na Geshemu, Mwarabu, waliposikia, wakatucheka na kutuzomea wakisema, “Ni kitu gani hiki mnachotenda? Je, mnataka kumwasi mfalme?”

20 Nikawajibu, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha katika kazi hii, nasi tulio watumishi wake tutaanza ujenzi. Lakini nyinyi hamna fungu wala haki wala kumbukumbu katika mji wa Yerusalemu.”

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13