Nehemia 6 BHN

Njama za kumwangamiza Nehemia

1 Kisha Sanbalati, Tobia, Geshemu, Mwarabu na adui zetu wengine, waliposikia kuwa tumemaliza ujenzi wa ukuta na kwamba hakuna mapengo yoyote (ingawa tulikuwa bado hatujaweka milango ya malango),

2 Sanbalati na Geshemu walituma ujumbe kwangu wakisema, “Na tukutane kwenye kijiji kimojawapo cha tambarare ya Ono.” Lakini walikusudia kunidhuru.

3 Basi, nikawapelekea wajumbe, nikisema, “Kazi ninayoifanya ni muhimu sana. Hivyo siwezi kuja kwenu ili kazi isije ikasimama.”

4 Waliendelea kunitaka niende kwao mara nne, lakini nikawapa jibu lilelile.

5 Mara ya tano, Sanbalati akanitumia barua ya hadhara kwa njia ya mjumbe wake.

6 Na barua yenyewe iliandikwa ifuatavyo:“Kuna habari zilizoenezwa miongoni mwa mataifa jirani, na Geshemu anathibitisha habari hizi, kuwa wewe pamoja na Wayahudi wenzako mnakusudia kuasi. Hii ndiyo sababu mnaujenga upya ukuta. Kulingana na habari hizo, wewe unakusudia kuwa mfalme wao.

7 Ili kuthibitisha wazo lako, umejiwekea manabii mjini Yerusalemu ili watangaze kuwa ‘Kuna mfalme katika nchi ya Yuda’. Taarifa hii ataarifiwa mfalme Artashasta. Hivyo nashauri wewe na mimi tukutane na kuzungumzia jambo hili.”

8 Nami nikampelekea ujumbe: “Hakuna jambo kama hilo. Habari hizo umezibuni wewe mwenyewe.”

9 Walifanya hivyo ili kututisha wakifikiri: “Hawataendelea na kazi, kwa hiyo, hakuna litakalotendeka.” Nikamwomba Mungu wangu nikisema, “Lakini sasa, ee Mungu, nakuomba unipe nguvu.”

10 Nilipokwenda nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya mwana wa Mehetabeli, ambaye hakuruhusiwa kutoka nyumbani, aliniambia, “Twende tukutane katika nyumba ya Mungu na milango yake tuifunge kwa sababu leo usiku wanakuja kukuua.”

11 Lakini mimi nikajiuliza moyoni, “Je, mtu kama mimi, ana haja ya kukimbia? Mtu kama mimi anahitaji kuingia hekaluni kusudi apate kuishi? Kamwe sitaingia hekaluni.”

12 Kwa bahati nzuri, nilingamua kuwa alikuwa hajatumwa na Mungu, bali alikuwa amekodishwa na Tobia na Sanbalati atangaze mabaya dhidi yangu.

13 Alikuwa amekodishwa kunitishia nami nifanye dhambi. Na kwa njia hii wangepata mwanya wa kuniharibia jina langu ili kushusha hadhi yangu.

14 Nikamwomba Mungu nikisema, “Ee Mungu, kumbuka yote waliyotenda Tobia na Sanbalati, hata yule Noadia, nabii mwanamke, na manabii wengine waliotaka kunifanya niogope.”

Kazi inakamilika

15 Basi, ukuta ulikamilika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli; nayo ilichukua muda wa siku hamsini na mbili.

16 Maadui zetu katika mataifa jirani, waliposikia kuwa kazi tumeimaliza, waliogopa na kuona aibu sana; kwani walijua hakika kuwa kazi hii ilikamilika kwa msaada wa Mungu wetu.

17 Wakati huu wote, viongozi wa Wayahudi walikuwa wakiandikiana na Tobia.

18 Wengi miongoni mwa Wayahudi walishirikiana naye kutokana na kiapo chao kwani alikuwa mkwe wa Shekania, mwana wa Ara. Zaidi ya yote, Yehohanani, mwanawe, alikuwa amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.

19 Pia wakanisimulia matendo mema ya Tobia, na habari zangu wakawa wanampelekea. Naye akawa ananiandikia barua ili kunitisha.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13