1 Kwenye hati yenye mhuri kulikuwapo majina ya Nehemia, mtawala wa mkoa, mwana wa Hakalia, na Sedekia;
2 Seraya, Azaria, Yeremia,
3 Pashuri, Amaria, Malkiya,
4 Hatushi, Shebania, Maluki,
5 Harimu, Meremothi, Obadia,
6 Danieli, Ginethoni, Baruku,
7 Meshulamu, Abiya, Miyamini,
8 Maazia, Bilgai na Shemaya.
9 Pia majina ya Walawi: Yeshua, mwana wa Azania, Binui, wazawa wa Henadadi, Kadmieli.
10 Na ndugu zao waliotia sahihi ni: Shebania, Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani,
11 Mika, Rehobu, Hashabia,
12 Zakuri, Sherebia, Shebania,
13 Hodia, Bani na Beninu.
14 Majina ya viongozi wa watu: Paroshi, Pahath-moabu, Elamu, Zatu, Bani,
15 Buni, Azgadi, Bebai,
16 Adoniya, Bigwai, Adini,
17 Ateri, Hezekia, Azuri,
18 Hodia, Hashumu, Bezai,
19 Harifu, Anathothi, Nebai,
20 Magpiashi, Meshulamu, Heziri,
21 Meshezabeli, Sadoki, Yadua,
22 Pelatia, Hanani, Anaya,
23 Hoshea, Hanania, Hashubu,
24 Haloheshi, Pilha, Shobeki,
25 Rehumu, Hashabna, Maaseya,
26 Ahia, Hanani, Anani,
27 Maluki, Harimu na Baana.
28 Sisi sote watu wa Israeli, makuhani, Walawi, wangoja malango, waimbaji, watumishi wa hekalu na watu wote waliojitenga na mataifa jirani kufuata sheria ya Mungu pamoja na wake zao, wana wao na binti zao, wote wenye maarifa na fahamu,
29 tunaungana na ndugu zetu, wakuu wetu, katika kula kiapo na kwamba tukivunja kiapo hiki tutaapizwa, na twaapa kuwa tutaishi kwa kufuata sheria ya Mungu ambayo aliitoa kwa njia ya Mose, mtumishi wake. Tena tutatii yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, anatuamuru, na kuwa tutashika maagizo yake na kufuata masharti yake.
30 Binti zetu hatutawaoza kwa watu wa nchi hii na wala wana wetu hawataoa kwao.
31 Ikiwa watu hao wanaleta bidhaa au nafaka kuuza siku ya Sabato, sisi hatutanunua siku hiyo wala siku nyingine yoyote iliyo takatifu. Mwaka wa saba hatutailima ardhi na madeni yote tutayafuta.
32 Tunajiwekea sheria kwamba kwa mwaka tutatoa theluthi moja ya shekeli kwa ajili ya gharama za huduma ya nyumba ya Mungu:
33 Mikate mitakatifu, sadaka za nafaka za kawaida, sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za siku za Sabato, sikukuu za mwandamo wa mwezi, sikukuu nyingine zilizowekwa, vitu vingine vitakatifu, sadaka za kuondoa dhambi, ili kuwafanyia upatanisho watu wa Israeli na kazi nyingine zozote za nyumba ya Mungu wetu.
34 Sisi sote, watu wote, makuhani na Walawi tutapiga kura kila mwaka ili kuchagua ukoo utakaoleta kuni za kuteketeza tambiko madhabahuni pa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama sheria ilivyo.
35 Tunaahidi kuleta kila mwaka malimbuko yetu ya mazao na ya matunda ya kila mti kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
36 Kwa kufuata ilivyoandikwa katika sheria kila mzaliwa wa kwanza wa kiume, katika nyumba zetu, atapelekwa katika nyumba ya Mungu wetu kwa makuhani wanaohudumu humo, pia tutapeleka kila mtoto wa kwanza wa kiume wa ng'ombe wetu, mbuzi wetu na kondoo wetu.
37 Kila unga wetu wa kwanza, matoleo yetu, matunda ya miti, divai na mafuta tutavileta kwa kuhani kwenye vyumba vya nyumba ya Mungu wetu. Tena tutaleta zaka zetu za mazao yetu kwa Walawi, kwani ndio wanaohusika na ukusanyaji wa zaka hizo katika vijiji vyetu.
38 Kuhani, mzawa wa Aroni, atakuwa na Walawi wanapopokea zaka. Halafu Walawi watapeleka sehemu ya kumi ya zaka zote zilizotolewa katika nyumba ya Mungu kwenye vyumba na ghala.
39 Watu wa Israeli na Walawi watayapeleka matoleo ya nafaka, divai na mafuta ya zeituni kwenye vyumba ambamo vyombo vya patakatifu vinatunzwa na ambamo makuhani, wangoja malango na waimbaji wana vyumba vyao. Na daima tutaijali nyumba ya Mungu wetu.