1 Lifuatalo ni simulizi la Nehemia, mwana wa Hakalia.Ikawa, nilipokuwa katika mji mkuu wa Susa, katika mwezi wa Kislevu wa mwaka wa ishirini,
2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akaja pamoja na baadhi ya watu toka nchini Yuda. Nikawauliza kuhusu Wayahudi wenzetu waliosalimika, yaani ambao hawakuhamishiwa Babuloni na kuhusu mji wa Yerusalemu.
3 Wao wakaniambia, “Wayahudi waliosalimika na kubaki katika mkoa ule, wako katika taabu na aibu. Ukuta wa mji wa Yerusalemu umebomolewa na malango yake yameteketea.”
4 Niliposikia hayo nilikaa chini na kulia, nikaomboleza kwa siku kadhaa. Nikafunga na kumwomba Mungu wa mbinguni,
5 nikisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbinguni, wewe u Mungu aliye mkuu na wa kutisha, unalishika agano lako na unawafadhili wale wakupendao na kuzishika amri zako.
6 Yasikilize kwa makini maombi yangu, na uniangalie mimi mtumishi wako, ninapokuomba kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli, usiku na mchana. Ninaungama dhambi za watu wa Israeli, tulizofanya mbele yako. Mimi pamoja na watu wa jamaa yangu tumefanya dhambi.