14 Tangu wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wa nchi ya Yuda kwa miaka kumi na miwili yaani tangu mwaka wa ishirini mpaka mwaka wa thelathini na mbili wa kutawala kwa mfalme Artashasta, sikula chakula kinachostahili kuliwa na mtawala, wala ndugu zangu hawakufanya hivyo.
15 Watawala walionitangulia walikuwa mzigo mzito kwa watu wakiwadai chakula na divai, mbali na kuwadai kuwalipa sarafu za uzito wa shekeli arubaini za fedha. Hata watumishi wao waliwadhulumu watu. Bali, mimi sikufanya hivyo, kwani nilimcha Mungu.
16 Nilikuwa na juhudi nyingi katika ujenzi mpya wa ukuta huu na kamwe sikujipatia hata shamba. Hata watumishi wangu wote walifanya kazi hii kwa bidii.
17 Zaidi ya hayo, kila siku niliwalisha watu 150, wakiwamo Wayahudi na maofisa, mbali na wale watu waliotujia toka mataifa jirani.
18 Kila siku, ili kuwalisha watu hao, nilichinjiwa dume mmoja na kondoo safi sita na kuku. Kila baada ya siku kumi nilitoa kwa wingi viriba vya divai. Lakini licha ya haya yote, kwa kuwa watu walikuwa na mzigo mzito wa kubeba kila siku, sikutaka posho ya ziada.
19 Sasa, ee Mungu wangu, kumbuka wema wangu wote niliowatendea watu hawa.