23 Lakini huyo mzee mwenye nyumba akatoka nje, akawaambia “Sivyo ndugu zangu; nawasihi msitende uovu huo. Huyu ni mgeni wangu, hivyo msimtendee ubaya huo.
24 Ninaye bado binti yangu ambaye ni bikira na yupo pia yule suria wa mgeni wangu. Niruhusuni niwatoe nje, muwachukue na kuwatendea kama mnavyotamani; lakini mtu huyu msimtendee jambo hilo la kipumbavu.”
25 Lakini wanaume hao hawakumsikiliza. Kwa hiyo Mlawi yule akamchukua suria wake na kumtoa kwao huko nje. Nao wakamchukua na kumnajisi usiku kucha mpaka asubuhi. Karibu na mapambazuko, wakamwacha aende zake.
26 Asubuhi, yule mwanamke akaja mpaka mlangoni mwa nyumba alimokuwa bwana wake, akaanguka chini hapo mlangoni na kukaa hapo mpaka kulipopambazuka kabisa.
27 Bwana wa mwanamke huyo alipoamka asubuhi, alifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aendelee na safari. Ghafla akamkuta suria wake amelala chini mlangoni, mikono yake ikishika kizingiti cha mlango.
28 Akamwambia, “Simama twende.” Lakini yeye hakujibu kitu. Akamchukua, akamweka juu ya punda wake na kumpeleka mpaka nyumbani kwake.
29 Alipofika nyumbani kwake akachukua kisu na kumkatakata yule suria vipande kumi na viwili. Kisha akavipeleka vipande hivyo katika maeneo yote ya nchi ya Israeli.