9 Hivi ndivyo tutakavyofanya kuhusu Gibea: Tutapiga kura namna ya kuwashambulia.
10 Tutachagua watu kumi katika kila watu mia moja wa Israeli, watu mia moja katika kila watu elfu moja, watu elfu moja katika kila watu elfu kumi. Hao watakuwa na jukumu la kuwaletea chakula wenzao watakaokuwa na kazi ya kuuadhibu mji wa Gibea katika nchi ya Benyamini kwa uhalifu wao na upotovu walioufanya katika Israeli.”
11 Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa moyo mmoja dhidi ya mji wa Gibea.
12 Watu wa makabila ya Israeli wakatuma wajumbe mpaka kila sehemu ya kabila la Benyamini, wakisema, “Je, ni uovu gani huu uliotukia miongoni mwenu?
13 Sasa tupeni hao watu mabaradhuli wa Gibea ili tuwaue na kutokomeza uovu huu kutoka Israeli.” Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwasikiliza ndugu zao, Waisraeli.
14 Basi walikusanyika huko Gibea kutoka katika kila mji wao, ili kupigana na Waisraeli.
15 Watu wa kabila la Benyamini walikusanya kutoka miji yao jeshi la watu 26,000 wenye kutumia silaha, nao wakazi wa mji wa Gibea wakakusanya watu 700 waliochaguliwa.