2 Basi, wakaenda mpaka Betheli wakakaa huko mbele ya Mungu hadi jioni. Wakapaza sauti na kulia kwa uchungu mwingi.
3 Wakasema “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limetukia hata tupungukiwe na kabila katika Israeli?”
4 Kesho yake watu waliamka mapema, wakajenga madhabahu, wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
5 Kisha wakaulizana, “Je, miongoni mwa makabila yote ya Israeli kuna kikundi chochote ambacho hakikuhudhuria mkutano uliofanyika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Walikuwa wamefanya kiapo kwamba mtu yeyote ambaye hatahudhuria mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa ni lazima auawe.
6 Lakini Waisraeli wakawaonea huruma ndugu zao wa kabila la Benyamini, wakasema, “Leo kabila moja la Israeli limeangamia.
7 Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wake hao wanaume wa kabila la Benyamini waliosalia? Maana tulikwisha apa kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hatutawapa binti zetu wawe wake zao!”
8 Wakataka kujua kama kulikuwa na kikundi chochote cha makabila ya Israeli ambacho hakikuhudhuria mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. Wakagundua kwamba hakuna mtu yeyote kutoka Yabesh-gileadi aliyekuja kwenye mkutano huo.