22 Ndipo Gideoni akatambua kwamba huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu; akasema, “Ole wangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu, maana nimemwona malaika wako uso kwa uso.”
23 Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Amani iwe nawe! Usiogope, hutakufa.”
24 Gideoni akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko na kuyaita, “Mwenyezi-Mungu ni Amani.” Madhabahu hiyo iko huko Ofra, mji wa Wabiezeri, mpaka leo.
25 Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Chukua fahali mmoja wa baba yako, fahali yule wa pili wa umri wa miaka saba. Bomoa madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako na kuvunja sanamu ya Ashera iliyo karibu nayo.
26 Halafu, unijengee mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, madhabahu nzuri juu ya mwinuko huu. Kisha unitolee sadaka ya kuteketezwa ya yule fahali wa pili ukitumia kuni za ile sanamu ya Ashera uliyoivunja.”
27 Basi, Gideoni akachukua watumishi wake kumi, akafanya kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Lakini kwa kuwa aliiogopa jamaa yake na watu wa mjini, badala ya kufanya hayo mchana, alifanya wakati wa usiku.
28 Wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema waliona madhabahu ya Baali na sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo vimeharibiwa. Yule fahali wa pili alikuwa ameteketezwa juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa mahali hapo.