1 Watu wa kabila la Efraimu wakamwuliza Gideoni, “Kwa nini umetutendea hivyo? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali.
2 Lakini Gideoni akawajibu, “Mambo niliyofanya mimi si kitu kabisa kama yakilinganishwa na yale mliyoyafanya nyinyi. Walichookota watu wa Efraimu baada ya mavuno ni chema na kizuri kuliko mavuno ya jamaa yangu ya Abiezeri.
3 Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia.
4 Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao.