3 Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia.
4 Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao.
5 Basi, akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni wenzangu hawa mikate maana wamechoka sana; nami bado ninaendelea kuwafuatia wafalme Zeba na Salmuna wa Midiani.”
6 Lakini viongozi wa Sukothi wakamwuliza, “Kwa nini tuwape mikate nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?”
7 Gideoni akawaambia, “Sawa, lakini Mwenyezi-Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mikononi mwangu, nitaichanachana miili yenu kwa miiba na mbigili za jangwani.”
8 Kutoka huko akawaendea watu wa Penueli, akawaomba namna ileile. Nao watu wa Penueli wakamjibu kama walivyomjibu watu wa Sukothi.
9 Gideoni akawaambia, “Nitakaporudi kwa amani nitaubomoa mnara huu.”