42 Kisha watachukua mawe mapya na kujenga mahali walipobomoa; nao wataipiga nyumba hiyo lipu upya.
43 “Ikiwa upele huo utatokea tena baada ya kutoa mawe hayo na kukwangua lipu na kuipiga lipu upya,
44 yapasa kuhani aje kuichunguza. Ikiwa upele umeenea katika nyumba hiyo, basi huo ni upele wa kufisha; nyumba hiyo ni najisi.
45 Nyumba hiyo ni lazima ibomolewe na mawe yake, miti yake na lipu vipelekwe mahali najisi nje ya mji.
46 Zaidi ya hayo, yeyote atakayeingia ndani ya nyumba hiyo wakati itakapokuwa imefungwa, atakuwa najisi mpaka jioni.
47 Yeyote anayelala katika nyumba hiyo au kulia chakula ndani yake, lazima ayafue mavazi yake.
48 “Lakini ikiwa baada ya kuikagua nyumba hiyo, kuhani ataona kuwa upele haujaenea baada ya kupigwa lipu, basi, kuhani atatangaza kuwa nyumba hiyo ni safi kwani upele umekwisha.