Walawi 15 BHN

Vitu najisi vya mwili

1 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose na Aroni,

2 “Waambieni Waisraeli hivi: Mwanamume yeyote akitokwa na usaha, usaha huo wamfanya kuwa najisi.

3 Na ufuatao ni mwongozo kuhusu najisi hiyo: Muda wote anapotokwa na usaha au usaha unapokuwa umezuiwa ndani yake, mtu huyo ni najisi.

4 Kitanda chochote atakacholalia au atakachokalia, kitakuwa najisi.

5 Mtu yeyote atakayegusa kitanda chake mtu huyo ni lazima ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

6 Mtu yeyote atakayekalia kitu chochote alichokalia huyo mtu mwenye kutokwa na usaha, ni lazima ayafue mavazi na kuoga; na atakuwa najisi hadi jioni.

7 Mtu yeyote atakayemgusa mtu atokwaye na usaha, lazima afue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

8 Mtu yeyote akitemewa mate na mtu anayetokwa usaha ni lazima mtu huyo aliyetemewa mate ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

9 Tandiko lolote la mnyama aliloketia mtu anayetokwa na usaha litakuwa najisi.

10 Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote alichokalia mtu huyo, atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote anayebeba kitu chochote kilichokuwa cha mtu huyo ni lazima ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

11 Mtu yeyote anayetokwa na usaha akimgusa mtu bila kusafisha kwanza mikono yake na kuoga, aliyeguswa atakuwa najisi mpaka jioni.

12 Chombo chochote cha udongo kilichoguswa na mtu anayetokwa na usaha ni lazima kivunjwe. Lakini chombo chochote cha mbao ni lazima kisafishwe kwa maji.

13 “Mwanamume yeyote anayetokwa na usaha akiponywa ugonjwa wake, ni lazima huyo mtu angoje siku saba kabla ya kuondolewa unajisi wake. Atayafua mavazi yake na kuoga kwa maji ya mtoni; naye atakuwa safi.

14 Siku ya nane, ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa mbele ya Mwenyezi-Mungu mlangoni mwa hema la mkutano na kumkabidhi kuhani.

15 Kuhani atawatoa hao, mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa na usaha.

16 “Kama mwanamume yeyote akitokwa na shahawa yake, ni lazima aoge mwili mzima kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

17 Vazi lolote lililodondokewa shahawa au ngozi yoyote iliyoguswa na shahawa hiyo ni lazima ioshwe kwa maji, na itakuwa najisi mpaka jioni.

18 Kama mwanamume akilala na mwanamke, akatokwa na shahawa, basi, ni lazima wote wawili waoge kwa maji, nao watakuwa najisi mpaka jioni.

19 “Mwanamke yeyote anapokuwa mwezini, atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Mtu yeyote atakayemgusa mwanamke huyo atakuwa najisi mpaka jioni.

20 Kitu chochote anacholalia au kukalia wakati yu najisi, kitakuwa najisi.

21 Mtu yeyote atakayegusa kitanda cha huyo mwanamke ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

22 Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote anachokalia mwanamke huyo ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

23 Mwanamume yeyote atakayegusa kitu chochote alicholalia au kukalia huyo mwanamke, atakuwa najisi mpaka jioni.

24 Kama mwanamume akilala na mwanamke huyo na damu ya huyo mwanamke ikamdondokea huyo mwanamume, basi, mwanamume huyo atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Kitanda chochote atakacholalia huyo mwanamume kitakuwa najisi.

25 “Kama mwanamke anatokwa na damu kwa muda wa siku nyingi kuliko ilivyo kawaida au anatokwa damu wakati usio wa majira yake ya kutokwa damu, basi, ataendelea kuwa najisi muda wote damu inapomtoka.

26 Kitanda chochote anacholalia wakati huo au kiti chochote anachokalia, kitakuwa najisi sawa kama wakati wa unajisi wake wa kutokwa damu.

27 Mtu yeyote atakayegusa vitu hivyo, atakuwa najisi na ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

28 Baada ya kukauka damu yake mwanamke huyo atangoja hadi siku saba ili kuwa safi; na baada ya muda huo atakuwa safi.

29 Siku ya nane atachukua hua wawili au makinda mawili ya njiwa na kumletea kuhani mlangoni mwa hema la mkutano.

30 Kuhani atamtoa mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mwanamke ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa damu.

31 “Ndivyo mtakavyowatahadharisha Waisraeli na unajisi wao, wasije wakaikufuru maskani yangu takatifu iliyo miongoni mwao wakiingia humo na unajisi wao; wakifanya hivyo watauawa.”

32 Hiyo ndiyo sheria kuhusu mwanamume anayetokwa na usaha na anayetokwa na shahawa na kuwa najisi.

33 Sheria hiyo yamhusu pia mwanamke anayetokwa damu na kuwa najisi. Sheria hiyo yamhusu mwanamume au mwanamke yeyote anayetokwa na chochote na pia yahusu mwanamume anayelala na mwanamke ambaye ni najisi.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27