Walawi 11 BHN

Wanyama najisi na wasio najisi

1 Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni,

2 “Wawaambie Waisraeli hivi:

3 Kati ya wanyama wote duniani, mmeruhusiwa kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.

4 Lakini msile mnyama yeyote ambaye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili, au ambaye kwato zake zimegawanyika lakini hacheui. Msile ngamia, kwani hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili. Kwenu huyo ni najisi.

5 Pelele msimle; yeye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika; kwenu huyo ni najisi.

6 Sungura msimle; yeye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika; kwenu huyo ni najisi.

7 Nguruwe msimle; ana kwato zilizogawanyika lakini hacheui; kwenu huyo ni najisi.

8 Kwa sababu wanyama hao ni najisi msile nyama yao wala msiguse mizoga yao.

9 “Samaki yeyote wa baharini au mtoni mwenye mapezi na magamba, mnaweza kumla.

10 Lakini chochote kinachoishi baharini au mitoni, ambacho hakina mapezi wala magamba, yaani viumbe vyote viendavyo majini na viumbe vingine vyote viishivyo majini ni najisi kwenu.

11 Viumbe hivyo vitakuwa daima najisi kwenu. Msile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao kwani ni najisi.

12 Chochote kinachoishi majini ambacho hakina mapezi na magamba ni najisi kwenu.

13 “Ndege wote wafuatao ni najisi kwenu; hivyo msile: Tai, furukombe, kipungu,

14 mwewe, aina zote za kozi,

15 aina zote za kunguru,

16 mbuni, kirukanjia, dudumizi, aina zote za kipanga,

17 bundi, mnandi, bundi kubwa,

18 mumbi, mwari, mderi,

19 korongo, aina zote za koikoi, hudihudi na popo.

20 “Wadudu wote wenye mabawa na waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu.

21 Lakini, baadhi ya wadudu wenye mabawa na wanakwenda kwa miguu minne ya kurukia ardhini mnaweza kula.

22 Hao ni: Kila aina ya nzige, kila aina ya senene, kila aina ya panzi na kila aina ya parare.

23 Lakini wadudu wengine wote wenye mabawa na miguu minne ni najisi kwenu.

24 “Kugusa wanyama fulanifulani humfanya mtu kuwa najisi; yeyote atakayegusa mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni.

25 Mtu akichukua sehemu ya mizoga yake atakuwa najisi mpaka jioni, na mavazi yake ni lazima yafuliwe.

26 Mtu yeyote akigusa mnyama mwenye kwato zilizogawanyika lakini hacheui, mtu huyo atakuwa najisi.

27 Wanyama wote waendao kwa vitanga vyao ingawa wana miguu minne, ni najisi kwenu; na yeyote atakayegusa mzoga wa mnyama kama huyo atakuwa najisi mpaka jioni.

28 Mtu yeyote anayebeba mzoga atakuwa najisi, naye atasafisha mavazi yake. Hao ni najisi kwenu.

29 “Viumbe vifuatavyo ni najisi kwenu: Kicheche, panya, kila aina ya mjombakaka,

30 guruguru, kenge, mijusi, goromwe, na kinyonga.

31 Hao wote ni najisi kwenu na yeyote atakayegusa mizoga yao, atakuwa najisi mpaka jioni.

32 Ikiwa mzoga wa viumbe hao unakiangukia kitu chochote, kiwe ni kifaa cha mbao au vazi au ngozi au gunia au chombo chochote kitumiwacho kwa kusudi lolote lile, chombo hicho kitakuwa najisi mpaka jioni. Ili kukifanya kiwe safi ni lazima kukiosha kwa maji.

33 Ikiwa mzoga wake umeangukia chombo cha udongo, basi, chochote kilicho ndani ya chombo hicho ni najisi na lazima chombo hicho kivunjwe.

34 Chakula au kinywaji chochote kilichokuwa ndani ya chombo hicho kitakuwa najisi.

35 Kila kitu ambacho sehemu ya mzoga imekiangukia, kitakuwa najisi. Ikiwa ni tanuri au jiko, ni lazima kivunjwe. Vitakuwa najisi navyo ni najisi kwenu.

36 Hata hivyo, kisima au chemchemi ya maji vitakuwa safi. Lakini chochote kinachogusa mzoga kitakuwa najisi.

37 Iwapo sehemu ya mzoga inaziangukia mbegu za kupanda, mbegu hizo hazitakuwa najisi.

38 Lakini ikiwa mbegu zimetiwa katika maji ili kuota na sehemu yoyote ya mzoga ikaziangukia, basi, mbegu hizo ni najisi kwenu.

39 “Iwapo mnyama yeyote mnayeruhusiwa kula, anakufa mwenyewe, yeyote atakayegusa mzoga wake, atakuwa najisi mpaka jioni.

40 Mtu yeyote akila nyama ya mzoga huo atafua mavazi yake na atakuwa najisi mpaka jioni. Na yeyote atakayebeba mzoga huo, atafua mavazi yake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

41 “Kiumbe chochote kitambaacho duniani ni najisi kwenu, kamwe msikile.

42 Chochote kiendacho kwa tumbo lake, chochote kiendacho kwa miguu yote minne au nyayo nyingi, naam, chochote kitambaacho, kamwe msikile kwa maana ni najisi kwenu.

43 Hivyo msije mkawa najisi kwa kula viumbe vitambaavyo na hivyo mkawa najisi.

44 Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi Mungu wenu, jiwekeni wakfu na kuwa watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu.

45 Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu; kwa hiyo muwe watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu.”

46 Hiyo basi, ndiyo sheria kuhusu wanyama, ndege na viumbe vyote hai ambavyo huishi majini na nchi kavu,

47 ili kupambanua kati ya kisicho najisi na kilicho najisi; kinachoweza kuliwa na kisichoweza kuliwa.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27