1 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie makuhani, wana wa Aroni, kwamba pasiwe na mtu yeyote miongoni mwao atakayejitia najisi kwa kugusa maiti ya watu wa jamaa yake,
2 isipokuwa kama ni maiti ya ndugu yake wa karibu, yaani mama yake, baba yake, mwanawe, binti yake, ndugu yake
3 au dada yake ambaye (aliye wa jamaa yake ya karibu), naye hajaolewa bado.
4 Yeye, akiwa mwenye madaraka katika jamaa yake, asijitie unajisi.
5 Wazawa wa Aroni kamwe wasijinyoe upara kuomboleza wala wasikate pembe za ndevu zao wala kujichanja chale mwilini.
6 Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao wala wasilikufuru jina la Mungu wao. Maana wao ndio wanaotolea zile sadaka anazopewa Mwenyezi-Mungu kwa moto yaani chakula cha Mungu. Basi, ni lazima wawe watakatifu.
7 Kwa kuwa kuhani amewekwa wakfu kwa Mungu wake, kamwe asioe kahaba, wala mwanamke asiye bikira wala aliyepewa talaka.
8 Utamtambua kuhani kuwa aliyewekwa wakfu, maana yeye ndiye anayetoa sadaka ya mkate wa Mungu wako; utamtambua kuwa mtakatifu, maana mimi Mwenyezi-Mungu ninayekuweka wewe wakfu, ni mtakatifu.
9 Binti wa kuhani yeyote akijitia unajisi kwa kufanya ukahaba, atateketezwa kwa moto kwani anamtia baba yake unajisi.
10 “Kuhani mkuu yeyote, kwa kuwa yeye ni mkuu kati ya ndugu zake, naye amemiminiwa mafuta ya kupaka kichwani pake, na kuwekwa wakfu ili ayavae mavazi matakatifu, asiache nywele zake kuwa ovyo wala asirarue mavazi yake kuomboleza.
11 Asikaribie maiti wala kujitia unajisi kwa maiti hata kama ni ya baba yake au ya mama yake.
12 Kwa kuwa amewekwa wakfu kwa kupakwa mafuta ya Mungu wake kichwani, basi asiondoke mahali patakatifu wala asipatie unajisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
13 Kuhani mkuu aweza tu kumwoa msichana ambaye ni bikira.
14 Haruhusiwi kuoa mwanamke mjane, mwanamke asiye bikira, wala kahaba. Ni lazima aoe bikira kutoka watu wake mwenyewe
15 asije akawatia unajisi watoto wake mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyemweka wakfu.”
16 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
17 “Mwambie Aroni hivi: Mzawa wako yeyote katika vizazi vyote vijavyo ambaye ana dosari mwilini, haruhusiwi kukaribia na kunitolea mimi Mungu wake sadaka ya mkate.
18 Mtu yeyote mwenye dosari sikaribie kunitolea sadaka: Awe kipofu, aliyelemaa, aliyeharibika uso, mwenye kiungo kirefu kuliko kawaida,
19 mwenye mguu au mkono ulioumia,
20 mwenye kibyongo, mtu mfupi kuliko kawaida, mwenye macho mabovu au ugonjwa wa ngozi, mwenye upele au towashi.
21 Mzawa yeyote wa kuhani Aroni mwenye kilema asikaribie kunitolea sadaka za kuteketezwa kwa moto; kwa vile ana kilema, basi, asikaribie kunitolea mimi Mungu mkate wangu.
22 Mtu huyo anaweza kula mkate wa Mungu wake, vitu vitakatifu na vile vitakatifu kabisa.
23 Lakini asilikaribie lile pazia wala ile madhabahu kwani ana dosari, asije akapatia unajisi mahali patakatifu; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu.”
24 Mose akamweleza Aroni na wanawe na Waisraeli wote mambo hayo yote.