6 Basi, kuhani atainyunyizia damu madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyoko mlangoni mwa hema la mkutano na kuyateketeza yale mafuta yawe harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
7 Kwa hiyo Waisraeli watakoma kabisa kutambikia yale majini, jambo ambalo limewafanya wakose uaminifu kwangu. Sharti hili ni la kudumu milele katika vizazi vyao vyote.
8 “Waambie kwamba mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli au mgeni anayeishi kati yao, anayetoa sadaka ya kuteketezwa au tambiko,
9 lakini haileti mbele ya mlango wa hema la mkutano ili kumtolea Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atatengwa na watu wake.
10 “Kama mtu yeyote wa jumuiya ya Israeli au mgeni anayeishi kati yao anakula damu yoyote, mimi nitamwandama mtu huyo aliyekula damu na kumtenga mbali na watu wake.
11 Itakuwa hivyo kwa sababu uhai wa kiumbe umo katika damu. Nimewaagiza kuitolea damu madhabahuni ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya roho zenu; kwa sababu damu hufanya upatanisho maana uhai umo katika damu.
12 Ndiyo maana nimewaagiza Waisraeli hivi: Mtu yeyote miongoni mwenu wala mgeni anayeishi kati yenu kamwe asile damu.