18 Kama mwanamume akilala na mwanamke aliye mwezini, wote wawili ni lazima watengwe na watu wao; huyo mwanamume amelala na mwanamke aliye na hedhi, na huyo mwanamke amelala na mwanamume akiwa na hedhi.
19 Usilale na dada ya mama yako wala na shangazi yako, maana hao ni jamaa yako wa karibu. Wote watendao hayo watawajibika kwa uovu wao.
20 Kama mtu akilala na mke wa baba yake, mkubwa au mdogo, anamwaibisha baba yake mkubwa au mdogo; wote wawili watawajibika kwa dhambi yao; wote wawili watakufa bila watoto.
21 Kama mwanamume akimwoa mke wa ndugu yake, anamwaibisha ndugu yake, huo ni unajisi; wote wawili watakufa bila watoto.
22 “Mnapaswa kushika na kutekeleza masharti na maagizo yangu yote; la sivyo nchi ile ambamo ninawapeleka itawatapika.
23 Msizifuate desturi za taifa ninalolifukuza mbele yenu; kwani waliyafanya hayo yote, nami nikawachukia sana.
24 Lakini, nimekwisha waambia, ‘Mtarithi nchi yao, mimi nawapa nchi hiyo muimiliki, nchi inayotiririka maziwa na asali.’ Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu niliyewatenga na mataifa mengine.