1 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2 “Mwambie Aroni na wanawe makuhani waviheshimu vitu ambavyo Waisraeli wameniwekea wakfu, wasije wakalikufuru jina langu takatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
3 Waambie hivi: Kama mmoja wa wazawa wenu katika vizazi vyenu vyote atavikaribia vitu vitakatifu ambavyo Waisraeli wameviweka wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu akiwa najisi, mtu huyo atatengwa nami. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
4 Mtu yeyote wa nasaba ya Aroni akiwa na ugonjwa wa ukoma au anatokwa usaha asile vitu vitakatifu mpaka atakapokuwa safi. Mtu yeyote akimgusa mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa,
5 au akigusa kiumbe chochote chenye kutambaa ambacho husababisha mtu kuwa najisi au mtu ambaye aweza kumtia unajisi wa aina yoyote ile,
6 mtu huyo, atakuwa najisi mpaka jioni na haruhusiwi kula vyakula vitakatifu mpaka hapo atakapokuwa ameoga.