33 Nitawatawanya nyinyi miongoni mwa watu wa mataifa na kuchomoa upanga dhidi yenu. Nchi yenu itakuwa ni ukiwa na miji yenu uharibifu.
34 “Nyinyi mtakapokuwa mikononi mwa adui zenu, hapo ndipo nchi itakapozifurahia sabato zake wakati itakapokuwa hali ya ukiwa. Nchi itapumzika na kufurahia sabato zake.
35 Kadiri itakapokuwa hali ya ukiwa itapata kiasi ambacho haikupata katika sabato zenu mlipokuwa mkiishi humo.
36 Na kwa baadhi yenu watakaosalimika nitawaletea woga mioyoni mwao, katika nchi ya adui zao hata jani linalopeperushwa litawakimbiza. Watakimbia kama mtu anayekimbia vita. Watakimbia na kuanguka hata kama hamna mtu anayewafukuza.
37 Wataangukiana ovyo kama mtu anayekimbia vita hata kama hamna anayewafukuza. Hamtakuwa na nguvu yoyote kuwakabili adui zenu.
38 Mtaangamia kati ya mataifa na nchi za adui zenu zitawameza.
39 Kama baadhi yenu wakisalimika katika nchi za adui zenu watadhoofika kwa sababu ya uovu wao; na kwa sababu ya uovu wa wazee wao.