5 Wazawa wa Aroni wataiteketeza madhabahuni pamoja na sadaka ya kuteketezwa iliyoko juu ya kuni; hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
6 “Kama sadaka hiyo ya kufanya amani unayomtolea Mwenyezi-Mungu ni kutoka kundi la kondoo au mbuzi, basi achaguliwe dume au jike asiye na dosari.
7 Kama mtu atatoa mwanakondoo kuwa sadaka yake, basi, atamtolea mbele ya Mwenyezi-Mungu,
8 akiweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama huyo na kumchinja mbele ya hema la mkutano. Makuhani wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu yake pande zake zote.
9 Kisha, kutoka katika sadaka hiyo ya amani anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto, atamtolea sehemu zifuatazo: Mafuta yake, mkia wenye mafuta mzima uliokatwa karibu kabisa na uti wa mgongo pamoja na mafuta yote yanayofunika matumbo na mafuta yote yaliyo kwenye matumbo,
10 zile figo mbili na mafuta yake pamoja na sehemu bora ya ini.
11 Kuhani ataviteketeza hivyo vyote juu ya madhabahu kama chakula anachotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto.