8 Nchi ya Tapua ilikuwa mali yake Manase, lakini mji wa Tapua, ambao ulikuwa mpakani, ulikuwa mali ya wazawa wa Efraimu.
9 Mpaka huo uliendelea hadi kijito cha Kana. Miji iliyokuwa kusini ya Kana ilikuwa ya Waefraimu hata ingawa ilikuwa katika nchi ya kabila la Manase. Halafu mpaka ukapita kaskazini ya kijito Kana na kuishia bahari ya Mediteranea.
10 Eneo la kusini lilikuwa la kabila la Efraimu na eneo la kaskazini lilikuwa la kabila la Manase, mpaka wake ukiwa bahari ya Mediteranea kwa upande wa magharibi. Kabila la Asheri lilikuwa kaskazini-magharibi ya eneo la Manase na kaskazini-mashariki lilikuwa kabila la Isakari.
11 Vilevile katika nchi ya kabila la Isakari na kabila la Asheri, kabila la Manase lilipatiwa miji ya Beth-sheani na Ibleamu pamoja na vijiji vyake, na miji ya Dori, En-dori, Taanaki na Megido pamoja na wakazi na vijiji vyake; na pia theluthi ya Nafathi.
12 Lakini wazawa wa Manase hawakuweza kuwafukuza wakazi wa miji hiyo, Wakanaani wakaendelea kuishi humo,
13 ingawa hata baada ya Waisraeli kuwa na nguvu zaidi, hawakuweza kuwafukuza ila tu waliwafanyisha kazi za kulazimishwa.
14 Watu wa kabila la Yosefu walimwendea Yoshua, wakamwambia, “Kwa nini umetugawia sehemu moja tu ya nchi sisi ambao Mwenyezi-Mungu ametubariki hata akatufanya tuwe wengi sana?”