1 Baada ya muda mrefu, Mwenyezi-Mungu aliwajalia Waisraeli amani kwa kuwaokoa na maadui zao pande zote. Wakati huo Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi.
2 Yoshua aliwaita Waisraeli wote pamoja na viongozi na wazee wao, waamuzi na maofisa, akawaambia, “Sasa mimi nimekuwa mzee wa miaka mingi.
3 Nyinyi mmeona mambo yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyoyatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye aliyewapigania.
4 Nchi za mataifa yaliyobaki na yale niliyoyaangamiza nimewagawieni ziwe mali ya makabila yenu, kutoka Yordani mpaka bahari ya Mediteranea, upande wa magharibi.
5 Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawaondoa mbele yenu na kuwafukuza kabisa, nanyi mtaimiliki nchi yao kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaahidi.
6 Kwa hiyo, muwe imara katika kuzingatia yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose, kamwe msiyaache.
7 Msishirikiane na mataifa haya yaliyobaki kati yenu. Msiitaje miungu yao wala msiape kwa majina ya miungu yao; msiitumikie wala msiisujudie.