12 Nilituma manyigu mbele yenu ambayo yaliwatimua wafalme wawili wa Waamori. Hamkufanya haya kwa kupania mapanga wala pinde zenu.
13 “Niliwapeni mashamba ambayo hamkuwa mmeyalima, na miji ambayo hamkuijenga ambamo sasa mnaishi, na kula matunda ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuipanda.
14 “Sasa, basi, mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa moyo mnyofu na uaminifu. Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliiabudu ngambo ya mto Eufrate na nchini Misri. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu.
15 Kama hamtaki kumtumikia Mwenyezi-Mungu, basi chagueni leo hii ni nani mtakayemtumikia: Kwamba ni miungu ile ambayo wazee wenu waliitumikia ngambo ya mto Eufrate, au miungu ya Waamori ambao sasa mnaishi nchini mwao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu.”
16 Hapo watu wakamjibu, “Hatutaweza kamwe kumwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu mingine.
17 Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ndiye aliyetutoa sisi pamoja na wazee wetu katika nchi ya Misri tulikokuwa watumwa, tukayaona kwa macho yetu wenyewe matendo ya ajabu aliyotenda. Akatulinda katika safari zetu zote na miongoni mwa watu wote ambao tulipita kati yao.
18 “Mwenyezi-Mungu alituondolea watu wote yaani Waamori wote waliokaa nchini. Kwa hiyo, nasi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, maana ndiye Mungu wetu.”