3 Basi, Yoshua akaondoka, pamoja na wanajeshi wake wote kwenda Ai. Akawachagua watu hodari 30,000 na kuwaambia watangulie wakati wa usiku.
4 Akawaamuru hivi: “Nyinyi mtauvizia mji kutoka upande wa nyuma. Msiende mbali na mji, bali muwe tayari wakati wote.
5 Mimi, pamoja na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji. Watu watakapotoka nje kuja kutukabili kama hapo awali, sisi tutawakimbia.
6 Nao wataendelea kutufuatia mpaka wawe mbali na mji wao, maana watafikiri wametutimua kama walivyofanya hapo awali. Sisi tutawaacha watufukuze.
7 Hapo, nyinyi mtatokea kutoka huko mlikokuwa mnavizia na kuuteka mji, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atautia mji huo mikononi mwenu.
8 Mkishauteka mji mtauteketeza kwa moto, kama vile Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hayo ndiyo maagizo mtakayofuata.”
9 Basi, Yoshua akawaambia waende mahali pao pa kuvizia; nao wakajiweka magharibi ya mji wa Ai kati ya mji wa Ai na Betheli. Lakini Yoshua alilala usiku huo katika kambi ya Waisraeli.