1 “Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu.
2 Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu.
3 Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri.
4 Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu,
5 bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’.
6 Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’”
7 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:“Amka, ee upanga!Inuka umshambulie mchungaji wangu;naam, mchungaji anayenitumikia.Mpige mchungaji na kondoo watawanyike.Nitaunyosha mkono wangu,kuwashambulia watu wadhaifu.