27 Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo.
28 Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa BWANA, akazishika pembe za madhabahu.
29 Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige.
30 Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu.
31 Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure.
32 Naye BWANA atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda.
33 Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa BWANA.