10 Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu.
11 Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.
12 Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji.
13 Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi BWANA.
14 Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, BWANA asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe.
15 Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.
16 Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.