16 Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA?
17 Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.
18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
19 Mikaya akasema, Sikia basi neno la BWANA; Nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.
20 BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
21 Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya.
22 BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.