30 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani.
31 Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.
32 Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga ukelele.
33 Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.
34 Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.
35 Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari.
36 Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.