1 Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti.
2 Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi wakaleta zawadi.
3 Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mamlaka yake kwenye mto wa Frati.
4 Daudi akampokonya magari elfu, na wapanda farasi saba elfu, na askari waendao kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia akawaweka.
5 Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu ishirini na mbili elfu.
6 Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.
7 Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu.