17 Daudi akamwambia Mungu, Je! Si mimi niliyeamuru watu wahesabiwe? Naam, mimi ndimi niliyekosa, na kufanya yaliyo maovu sana; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako, nakusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya babangu; wala si juu ya watu wako, hata wao wapigwe.
18 Ndipo huyo malaika wa BWANA akamwamuru Gadi kwamba amwambie Daudi, ya kuwa Daudi akwee, akamwinulie BWANA madhabahu katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.
19 Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, alilolinena kwa jina la BWANA.
20 Arauna alipogeuka, na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Arauna alikuwa akipura ngano.
21 Basi Daudi alipokuwa akimjia Arauna, Arauna akatazama, akamwona Daudi, akatoka katika kile kiwanja, akamsujudia Daudi kifulifuli hata nchi.
22 Ndipo Daudi akamwambia Arauna, Unipe mahali pa kiwanja hiki, ili kwamba nimjengee BWANA madhabahu hapa; kwa thamani yake kamili utanipa; ili kwamba tauni izuiliwe katika watu.
23 Arauna akamwambia Daudi, Ujitwalie, na bwana wangu mfalme na afanye yaliyo mema machoni pake; tazama, ng’ombe kwa sadaka za kuteketezwa, na vyombo vya kupuria kwa kuni, na ngano kwa sadaka ya unga, nazitoa; zote nazitoa.