1 Ikawa, baada ya kufa kwake Ahabu, Moabu wakawaasi Israeli.
2 Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu.
3 Lakini malaika wa BWANA akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni?
4 Basi sasa, BWANA asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.
5 Wale wajumbe wakarudi, na mfalme akawaambia, Mbona mmerudi?
6 Wakamwambia, Mtu alitokea, akaonana nasi, akatuambia, Enendeni, rudini kwa mfalme yule aliyewatuma, mkamwambie, BWANA asema hivi Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi kwa ajili ya hayo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa.
7 Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani?