1 Katika mwaka wa kumi na saba wa Peka mwana wa Remalia Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa BWANA Mungu wake, kama Daudi babaye.
3 Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.
4 Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi.
5 Hapo ndipo akakwea Resini mfalme wa Shamu pamoja na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli juu ya Yerusalemu ili wapigane; wakamhusuru Ahazi, ila hawakuweza kumshinda.
6 Wakati huo Resini mfalme wa Shamu akawarudishia Washami Elathi, akawafukuza Wayahudi kutoka Elathi; nao Washami wakaja Elathi, wakakaa humo hata leo.
7 Basi Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akasema, Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia.
8 Ahazi akatwaa fedha na dhahabu iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, akazipeleka kwa mfalme wa Ashuru kuwa zawadi.
9 Na huyo mfalme wa Ashuru akamsikia; mfalme wa Ashuru akapanda juu ya Dameski, akautwaa, akawahamisha watu wake mateka mpaka Kiri, akamwua Resini.
10 Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote.
11 Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski.
12 Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake.
13 Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu.
14 Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za BWANA, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya BWANA, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake.
15 Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie.
16 Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi.
17 Mfalme Ahazi akakata papi za matako, akaliondoa lile birika juu yake; akaitelemsha ile bahari itoke juu ya ng’ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe.
18 Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya BWANA, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru.
19 Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
20 Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.