1 Basi Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke, ambaye alimfufulia mwanawe, akasema, Ondoka, ukaende wewe na jamaa yako, ukae hali ya kigeni utakakoweza kukaa; kwa sababu BWANA ameiita njaa; nayo itakuja juu ya nchi hii muda wa miaka saba.
2 Akaondoka yule mwanamke, akafanya kama alivyosema mtu wa Mungu; akaenda, yeye na jamaa yake, akakaa katika nchi ya Wafilisti miaka saba.
3 Ikawa miaka saba ilipoisha, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti; akatokea amlilie mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.
4 Basi mfalme alikuwa akizungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, akinena, Uniambie, nakusihi, mambo makuu yote aliyoyafanya Elisha.
5 Ikawa, alipokuwa katika kumwambia mfalme jinsi alivyomfufua mtu aliyekufa, tazama, huyo mwanamke aliyemfufulia mwanawe, alimlilia mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Gehazi akasema, Bwana wangu mfalme, huyu ndiye mwanamke, na huyu ndiye mwanawe, ambaye Elisha alimfufua.
6 Na mfalme alipomwuliza yule mwanamke, yeye akamweleza. Basi mfalme akamtolea akida, akasema, Mrudishie yote aliyokuwa nayo, na mapato yote ya shamba lake tangu siku aliposafiri, hata leo.
7 Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa.
8 Mfalme akamwambia Hazaeli, Chukua zawadi mkononi mwako, ukaende ili kumlaki yule mtu wa Mungu, ukamwulize BWANA kwa kinywa chake, kusema, Je! Nitapona ugonjwa huu?
9 Basi Hazaeli akaenda kumlaki, akachukua zawadi mkononi mwake, za kila kitu chema kilichopatikana Dameski, kiasi cha mizigo ya ngamia arobaini, akaenda, akasimama mbele yake akasema, Mwana wako Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, amenituma kwako, kusema, Je nitapona ugonjwa huu?
10 Elisha akamwambia, Enenda, ukamwambie, Bila shaka utapona; lakini BWANA amenionyesha ya kwamba bila shaka atakufa.
11 Akamkazia macho hata akatahayari; na yule mtu wa Mungu akalia machozi.
12 Hazaeli akasema, Bwana wangu analilia nini? Akajibu, Kwa sababu nayajua mabaya utakayowatenda wana wa Israeli; utazichoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, utawaseta-seta watoto wao wachanga na wanawake wao wenye mimba utawapasua.
13 Hazaeli akasema, Lakini mimi mtumwa wako ni nani, mimi niliye mbwa tu, hata nifanye jambo hili kubwa? Elisha akajibu, BWANA amenionyesha ya kwamba wewe utakuwa mfalme juu ya Shamu.
14 Ndipo akamwacha Elisha, akarudi kwa bwana wake; naye akamwambia, Elisha alikuambiaje? Akajibu, Aliniambia ya kuwa bila shaka utapona.
15 Ikawa siku ya pili yake, akatwaa tandiko la kitanda, akalichovya katika maji, akalitandaza juu ya uso wake, hata akafa. Na Hazaeli akatawala badala yake.
16 Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, [Yehoshafati alipokuwa mfalme wa Yuda], alianza kutawala Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.
17 Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu.
18 Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA.
19 Walakini BWANA hakupenda kuiharibu Yuda, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, kama alivyomwahidia akasema, kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote.
20 Zamani zake, Edomu wakaasi mkononi mwa Yuda, wakajifanyia mfalme.
21 Basi akaenda Yehoramu mpaka Sairi, na magari yake yote pamoja naye. Akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na maakida wa magari; na watu wakakimbilia hemani kwao.
22 Hivyo Edomu wakaasi mkononi mwa Yuda hata leo. Na Libna wakaasi zamani zizo hizo.
23 Na mambo yote ya Yehoramu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
24 Akalala Yehoramu na baba zake, akazikwa pamoja na baba zake mjini mwa Daudi; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.
25 Katika mwaka wa kumi na mbili wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
26 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri mfalme wa Israeli.
27 Akaiendea njia ya nyumba ya Ahabu, akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa alikuwa mkwe wa jamaa ya Ahabu.
28 Akaenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu, huko Ramoth-gileadi; nao Washami wakamtia Yoramu jeraha.
29 Akarudi Yoramu mfalme, auguzwe katika Yezreeli jeraha walizotia Washami huko Rama alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli, kwa sababu alikuwa hawezi.