1 Ikawa, hapo BWANA alipopenda kumpandisha Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha.
2 Eliya akamwambia Elisha, Tafadhali, kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Betheli.
3 Elisha akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni.
4 Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko.
5 Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni.
6 Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili.
7 Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani.
8 Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu.
9 Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.
10 Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati.
11 Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.
12 Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.
13 Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.
14 Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.
15 Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.
16 Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume.
17 Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone.
18 Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende?
19 Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza.
20 Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea.
21 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza.
22 Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.
23 Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa!
24 Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la BWANA. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.
25 Akatoka huko akaenda mlima wa Karmeli, na toka huko akarudi mpaka Samaria.