3 Ila mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
4 Yoashi akawaambia makuhani, Fedha yote ya vitu vitakatifu iliyoletwa nyumbani mwa BWANA, fedha ya matumizi, fedha ya watu kadiri alivyoandikiwa kila mtu, na fedha yote iliyoletwa kama mtu ye yote aonavyo moyoni mwake kuileta nyumbani mwa BWANA,
5 makuhani na waitwae, kila mtu kwa hao awajuao; nao watatengeneza palipobomoka nyumbani, kila mahali palipoonekana pamebomoka.
6 Lakini ikawa, mwaka wa ishirini na tatu wa mfalme Yoashi, makuhani walikuwa hawajatengeneza mabomoko ya nyumba.
7 Ndipo mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani, na makuhani wengine, akawauliza, Mbona hamtengenezi mabomoko ya nyumba? Basi sasa msipokee tena fedha kwa hao mwajuao, lakini itoeni kwa ajili ya mabomoko ya nyumba.
8 Nao makuhani wakakubali kwamba wasipokee fedha kwa watu, wala wasitengeneze mabomoko ya nyumba.
9 Lakini Yehoyada kuhani akatwaa kasha, akatoboa tundu katika kifuniko chake, akaliweka karibu na madhabahu, upande wa kuume mtu aingiapo nyumbani mwa BWANA; na makuhani, waliolinda mlangoni, wakatia ndani yake fedha yote iliyoletwa nyumbani mwa BWANA.