5 BWANA akampiga mfalme, akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee. Na Yothamu mwana wa mfalme alikuwa juu ya nyumba, akiwahukumu watu wa nchi.
6 Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, nayo yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
7 Uzia akalala na babaze; wakamzika pamoja na babaze mjini mwa Daudi; na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake.
8 Katika mwaka wa thelathini na nane wa Uzia mfalme wa Yuda Zekaria mwana wa Yeroboamu akatawala juu ya Israeli katika Samaria miezi sita.
9 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA kama walivyofanya babaze; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
10 Na Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya fitina juu yake, akampiga mbele ya watu, akamwua, akatawala mahali pake.
11 Basi mambo yote ya Zekaria yaliyosalia, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.